Qari wa Lebanon: Kusoma na Kuhifadhi Qur’ani huleta baraka na mafanikio
Mashhad, Iran – Houra Haidar Hamza, ambaye aliwakilisha Lebanon katika kipengele cha usomaji (qiraa) kwenye Mashindano ya 41 ya Kimataifa ya Qur’an Tukufu ya Iran na kushika nafasi ya tatu, alisema kuwa kusoma na kuhifadhi Qur’ani si tu kunaboresha tabia ya mtu, bali pia huleta baraka na mafanikio maishani, huku kikiwa na athari chanya kwa mtu binafsi na jamii inayomzunguka.
Akizungumza na IQNA, qari huyo mwenye umri wa miaka 23 alisema:
Nilisomea hisabati katika chuo kikuu, lakini sikupendelea kuendelea katika taaluma hiyo na badala yake nikajielekeza kwenye Qur’an Tukufu. Alhamdulillah, niliweza kupiga hatua kubwa ndani ya miaka mitatu. Kwa sasa, mimi ni mwalimu wa Qur’an katika jiji la Karbala na ninafundisha katika *haramu ya Imam Hussein (AS).”
Uzoefu Wake Katika Mashindano ya Kimataifa
Houra alisema kuwa hii ni mara yake ya kwanza kushiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’an nchini Iran.
"Nimewahi kushiriki katika mashindano mengine ya kimataifa, kama yale yaliyofanyika Brazil, lakini yote yalifanyika mtandaoni. Nilishinda nafasi ya kwanza katika mashindano ya Brazil."
Alipoulizwa kuhusu kiwango cha mashindano haya na nafasi ya wasomaji wa kike wa Qur’an nchini Iran, alieleza:
"Kiwango cha wasomaji wa kike wa Qur’an nchini Iran kinaonyesha umakini na kujitolea kwa wananchi wa Iran kwa Qur’an Tukufu, pamoja na ukuaji wa ustadi wa Kiquran nchini humo. Kuhusu kiwango cha mashindano haya, ni cha juu sana, hasa ikizingatiwa kuwa washiriki wote ni vipaji vya juu kutoka nchi mbalimbali, na katika hatua za awali, walichaguliwa wasomaji na wahifadhi bora kutoka kila nchi."
Mashhad Kama Mwenyeji wa Mashindano
Kuhusu jiji takatifu la Mashhad kuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka huu, alisema kuwa ni hatua nzuri sana.
"Ni kwa baraka za Mwenyezi Mungu na ukarimu wa Imam Ridha (AS) tumekuja mahali hapa patakatifu. Natumai kuwa mashindano yajayo pia yatafanyika hapa, kwani yanatupa nguvu chanya ya kuendelea katika njia hii."
Nafasi ya Mashindano ya Qur’an Katika Kuhamasisha Vijana
Alipoulizwa kuhusu mchango wa mashindano haya kwa vijana, alieleza:
Mashindano ya Qur’ani yanaweza kuwa utangulizi wa kutekeleza mafundisho ya Qur’ani Tukufu. Yanawahamasisha watu kuhifadhi na kusoma Qur’an, jambo ambalo hujenga nafsi zenye mwelekeo wa Kiquran ndani ya jamii na kuhakikisha utekelezaji wa amri za Mwenyezi Mungu."
Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Iran
Mashindano haya huandaliwa kila mwaka na Shirika la Awqaf na Misaada ya Kiutu la Iran kwa lengo la kuendeleza utamaduni na maadili ya Kiquran miongoni mwa Waislamu na kuonyesha vipaji vya wasomaji na wahifadhi wa Qur’ani.
Hatua ya mwisho ya toleo la 41 ilihitimishwa siku ya Ijumaa mjini Mashhad, ambapo washindi katika vipengele tofauti walitangazwa na kutunukiwa tuzo.